05/06/2026
SAFARICOM, KCB NA NMB ZAONGOZA MFUKO WA UWEKEZAJI WA SOKO LA HISA, AFRIKA MASHARIKI
Wawekezaji wa Afrika Mashariki wanaendelea kuweka dau kubwa kwenye sekta ya benki na mawasiliano, huku kampuni ya simu ya Kenya, Safaricom, ikiongoza orodha ya uwekezaji mkubwa zaidi katika mfuko wa hisa wa kikanda (ETF) kwa asilimia 18.8 ya mali zote za mfuko.
Kwenye takwimu hizo zilizotoka tarehe 29 Mei, inaonesha benki ya KCB ikifuatia, kwa asilimia 14.99 na NMB Bank kwa asilimia 10.69.
Takwimu hizo zinaonyesha wawekezaji wanaendelea kuvutiwa na kampuni zinazotengeneza faida thabiti, kulipa gawio na kuwa na nafasi kubwa katika uchumi wa Afrika Mashariki.
Safaricom imeendelea kuimarika baada ya kutangaza faida ya zaidi ya TShs trilioni 1.8 (KES bilioni 100) na gawio kubwa zaidi katika historia yake, hatua iliyoongeza imani ya wawekezaji katika hisa hiyo.
Kwa upande wa benki, KCB, NMB, CRDB na taasisi nyingine za kifedha zimebeba karibu nusu ya uwekezaji wote wa mfuko huo, ishara kuwa wawekezaji wanaamini ukuaji wa huduma za kifedha na mikopo katika ukanda huu bado una nafasi kubwa ya kimaendeleo.
Kenya inaongoza kwa asilimia 49.29 ya uwekezaji wote wa mfuko, huku Tanzania ikifuata kwa asilimia 35.58. Uganda ina asilimia 10.17 na Rwanda asilimia 4.96.
Sekta ya benki pekee imechukua asilimia 43.79 ya uwekezaji wote, ikifuatiwa na mawasiliano kwa asilimia 27.91.