10/04/2026
Leo kupitia UjuziKazi, tumeamua kukujuza kwa kina kuhusu hatua mpya ya binadamu kuelekea MWEZINI kupitia mpango wa NASA unaoitwa Artemis II. ⤵️
*️⃣Kwa mujibu wa taarifa rasmi za NASA, safari hii ya kihistoria imefanikiwa kuufikia mwezi, mnamo April 2026, kwa namna ya kipekee zaidi ambapo wanaanga wamefanya mzunguko wa kuuzunguka mwezi (flyby mission) badala ya kutua. Hii ni hatua muhimu sana katika maandalizi ya safari za baadaye za kutua mwezini, na hii inatuthibitisha kwasasa kuwa dunia inaingia katika enzi mpya ya uchunguzi wa anga.
*️⃣Safari ya Artemis II ilizinduliwa rasmi tarehe 1 Aprili 2026 ikiwa na wanaanga wanne ambao ni Reid Wiseman, Victor Glover, Christina Koch na Jeremy Hansen. Safari hii ya siku kumi imelenga kufanya majaribio muhimu ya mifumo ya spacecraft, pamoja na kukusanya taarifa zitakazosaidia safari zijazo. Tarehe 6 Aprili 2026, wanaanga hao walifika umbali wa maili 252,756 kutoka duniani, wakivunja rekodi iliyowekwa mwaka 1970 na misheni ya Apollo 13. Safari inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 10 Aprili 2026 kwa kutua katika Bahari ya Pasifiki karibu na San Diego.
*️⃣Ni muhimu kuelewa kuwa licha ya mafanikio haya, misheni hii haikuhusisha kutua mwezini. NASA imepanga utekelezaji wa mpango wake kwa hatua, ambapo Artemis III itahusisha majaribio ya kuunganisha vyombo vya anga bila kutua mwezini. Hatua ya kurejea rasmi mwezini inatarajiwa kufanyika kupitia Artemis IV, ambayo inalenga kuwa safari ya kwanza ya binadamu kutua mwezini tangu mwaka 1972. Baada ya hapo, Artemis V inatarajiwa kuanza maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya kudumu mwezini.
*️⃣Safari hii ina umuhimu mkubwa kisayansi na kiuchumi kwa sababu inaashiria mwanzo wa uchumi mpya unaojulikana k**a space economy, ambapo nchi na makampuni binafsi yanaanza kuwekeza katika rasilimali na teknolojia za anga. Pia, ni mwendelezo wa mafanikio yaliyoanza kupitia Apollo Program, lakini safari hii inalenga zaidi uendelevu na uwepo wa muda mrefu wa binadamu nje ya dunia.
Kwa mtazamo wa UjuziKazi, mafanikio haya yanafunza kuwa maendeleo makubwa yanahitaji mchakato wa hatua kwa hatua unaojumuisha majaribio, tathmini na maboresho kabla ya kufikia lengo kuu.